Dodoma. Mpambano mkali wa kuwania nafasi ya
kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM sasa umeanza rasmi baada ya
Kamati Kuu ya chama hicho tawala kuwaweka huru makada sita waliokuwa
wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za
uchaguzi.
Kufunguliwa kwa makada hao, ambao baadhi yao
wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na chama hicho, kumekuja wakati CCM
ikikabiliwa na tishio la kutokea mgawanyiko mkubwa, hasa kutokana na
baadhi ya kambi kuituhumu sekretarieti kuwa inabagua baadhi ya wagombea.
Makada waliofungiwa tangu Februari, 2014 kwa kosa
la kuanza kampeni mapema ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye
na Edward Lowassa, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Monduli.
Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa
Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia), na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Baadhi ya wanachama wa CCM, hasa wajumbe wa
Halmashauri Kuu, walianza kumiminika nyumbani kwa makada hao mara baada
ya kupata taarifa za kuondolewa kwa adhabu hiyo, wengi wakionekana
kwenda kumpongeza Lowassa.
Kufunguliwa kwa makada hao ni mwanzo wa
kinyang’anyiro kikali cha kuwania kumrithi Jakaya Mrisho Kikwete kwenye
nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe na dalili zote za
kuwapo kwa vita kali zilianza mara moja jana baada ya kutangazwa kwa
uamuzi huo.
Post a Comment